WILAYA YA KIBAHA

Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha iko umbali wa kilometa 40 toka Jiji la Dar es salaam kando kando ya barabara kuu iendayo Morogoro. Halmashauri ya Wilaya inapatikana kati ya latitudi 6-8 Kusini mwa Ikweta na Longitudi 38.0 hadi 39.05 Mashariki. Kaskazini inapakana na Wilaya ya Bagamoyo, na Kusini inapakana na Wilaya ya Kisarawe, upande wa Mashariki inapakana na Halmashauri ya Mji wa kibaha, Upande wa Magharibi inapakana na Wilaya ya Bagamoyo na Wilaya ya Morogoro.

UTAWALA NA ENEO

Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ina jumla ya Tarafa 2 na Kata 14. Tarafa ni Mlandizi na Ruvu,Kata zake ni Kwala, Ruvu, Magindu, Mlandizi, Soga, Janga, Kilangalanga, Gwata, Bokomnemela, Dutumi, Kikongo, Kawawa, Mtongani, na Mtambani. Ikiwa na jumla ya Vijiji 25 na Vitongoji 100. Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ina eneo la ukubwa wa Hekta 124,217.755 sawa na kilometa za mraba 1992.18

HALI YA KIUCHUMI NA MAENDELEO

Halmashauri ya Wilaya Kibaha ina wakazi wachache waliosambaa katika maeneo mbalimbali isipokuwa Mji wa Mlandizi wenye wakazi wengi. Mji wa Mlandizi unakua haraka ukiwa na watu wa Tabaka mbalimbali na tamaduni zinazotofautiana. Ukaribu wake kutoka Mji Mkuu wa kibiashara Dar es Salaam unachangia kwa kiasi kikubwa. Mabadiliko ya kijamii na kiutamaduni hasa kutoka nchi za Kimagharibi.

Mlandizi inazo Taasisi nyingi za Umma na Binafsi zinazosaidia kutoa ajira kwa wakazi.  Hizi ni pamoja na shule za Msingi na Sekondari, JKT na Idadi kubwa ya wafanyabiashara kama maduka ya jumla, rejareja, migahawa, mama lishe vilabu vya pombe za kienyeji, viwanda vidogo kama upasuaji wa mbao, ushonaji, usagishaji n.k.

Shughuli za kiuchumi katika Halmashauri ya wilaya Kibaha ni kilimo, ufugaji ukiendeshwa zaidi na makabila ya Kimasai na Mang’ati hususani katika Kata za Kwala na Magindu. Ipo idadi ndogo ya wakazi wanaoendesha ufugaji wa kisasa wa kuku na ng’ombe wa maziwa. Mazao makuu ya kilimo ni Korosho, Ufuta, Machungwa, kilimo cha mbogamboga kama Matango, Nyanya, Pilipilli, Bilinganya, Matikiti maji n.k, kwa asilimia kubwa kilimo hiki hufanyika katika Bonde la Mto Ruvu. Mazao ya chakula ni pamoja na Mhogo, Mpunga, Mtama na Mahindi.

 

Shughuli za kilimo kwa kiasi kikubwa ni kwaajili ya kujikimu kwa chakula, ni watu wachache tu, hususani Mlandizi wako waajiriwa katika Taasisi za Umma na Binafsi kwa shughuli hii. Baadhi ya wakazi wanajishughulisha na uvunaji wa mazao ya Misitu kwa ajili ya ujenzi, kuni na uchomaji mkaa, kwa kiwango kidogo pia hujishughulisha na ufugaji na uvunaji wa mazao ya nyuki. Huduma za jamii zinazopatikana ni Afya, Elimu, Maji na Barabara. Mafanikio yote haya ni juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya Kibaha.

Humphrey Makussa

Mwanahabari

WANT TO CONNECT?