• By Humphrey Makussa

DC KIBAHA ASHUGHULIKIA MGOGORO SUGU WA ARDHI ZEGELENI

Mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu katika eneo la Zegereni wilayani Kibaha hatimaye umeshughulikiwa na Mkuu wa wa wilaya ya Kibaha Mhe. Eng. Martin Ntemo ambaye alifika katika eneo hilo na kukutana na makundi yanayosigana.


Awali akizungumza na wananchi wa eneo hilo DC Ntemo alibainisha kuwa, ziara ambazo ziko katika ratiba yake kwa wakati huu ni za kushughulikia masuala ya elimu, kuhakikisha wanafunzi waliofaulu darasa la saba wamejiunga na kidato cha kwanza na wale wanaoanza darasa la kwanza wanapata shule na kuanza masomo kikamilifu. ‘Mgogorö wenu ambao umekua na viashiria vya uvunjifu wa amani, umenilazimisha kukatisha ziara za kusimamia masuala ya elimu ili nikutane nanyi na kuhakikisha kuwa tunahitimisha suala hili’ alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.


Baada ya kusikiliza pande zinazosigana kuhusu umiliki wa ardhi ya Zegereni Eng. Ntemo alisema, kimsingi mgogoro huo haumhusu mwekezaji anayemiliki eneo hilo bali ni mgogoro baina ya waliovamia katika shamba hilo la mwekezaji. Hata hivyo, ilielezwa kuwa maongezi yamekwisha fanywa na mwekezaji na kukubaliana kuwa wananchi hao wataendelea kukaa katika maeneo wanayoishi kwa sasa. Jumla ya ekari 250 zimetengwa kutoka katika shamba hilo ili zipimwe na kugawiwa kwa wananchi hao pamoja na wengine watakaoomba kupitia Ofisi ya Mkurugenzi ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha.


Akiwa ameandama na Kamati nzima ya Usalama ya Wilaya, Mkurugenzi wa Mji wa Kibaha na Wataalamu mbalimbali, Mhe. Ntemo aliwatoa hufu wanakijiji hao kwa kuwahakikishia kuwa, upimaji katika eneo hilo utafanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha. Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo wale wote wanaoishi au waliuziwa ardhi katika eneo hilo, watawasilisha nyaraka zao kuonyesha uhalali wa umiliki au mauziano yaliyofanyika na orodha kamili itahakikiwa kabla ya ugawaji kuanza kwa lengo la kuepusha mamluki kuingia katika zoezi hilo.


Aidha, amewataka viongozi wa kijiji akiwepo Diwani, Mwenyekiti wa Mtaa na Mtendaji kuwa na utaratibu wa kufanya vikao na wananchi ili kupeana taarifa sahihi pale vikao vya maamuzi vinapofanyika ili kuepusha migongano isiyo ya lazima. Mhe. Martin Ntemo alihitimisha kwa kuwaagiza viongozi hasa wa Kata na Vijii kujenga tabia ya kufanya vikao na kumaliza migogoro yao wenyewe.Mkuu wa wilaya ya Kibaha Mhe. Martin Ntemo akisisitiza kuwepo kwa maelewano chanya baina ya wakazi wa Zegereni na viongozi wa serikali ya mtaa ili kuleta amani na kuepuka

migogoro isiyo ya lazima.

12 views
RECENT POST