• By Humphrey Makussa

DC NTEMO AAGIZA HALMASHAURI YA WILAYA NA TAASISI YA HIFADHI YA BAHARI MAFIA KUMALIZA TOFAUTI ZAO

Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhandisi Martin Ntemo hivi karibuni ameitembele taasisi ya Hifadi ya Bahari na Meneo Tengefu ya Kisiwa cha Mafia (HIBAMA) ili kujionea utekelezaji wa shughuli ambazo taasisi hiyo inazifanya.

Ziara hiyo ya Mkuu wa Wilaya ni sehemu ya ratiba ambayo anaitekeleza tangu alipowasili Kisiwani humo mwishoni mwa mwezi Juni 2021 mara baada ya kuteuliwa akitokea wilaya ya Kibaha, ambapo anazitembelea taasisi mbali mbali za Serikali zinazoendesha shughuli zao wilayani humo.

Hata hivyo, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa taasisi ya HIBAMA, Mkuu huyo wa wilaya alishangaa kuwepo na taarifa za mgongano wa kimaslahi kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Mafia na Taasisi hiyo ya Hifadi ya Bahari Mafia kiasi cha kusababisha kulegalega kwa usimamizi wa hifadhi hiyo kwa maelezo kuwa kumekuwepo na vikwazo vingi kutoka kwa viongozi hasa wa Halmashauri ya Wilaya na matamshi yanayoshabikia kuendelea kwa uvamizi katika hifadhi hiyo.

Hifadhi hii iliyoanzishwa mwaka 1995 inasimamia eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 822 na inajivunia kukusanya mapato yanayokadiriwa kuongezeka kutoka Shilingi 482 milioni mwaka 2014/15 hadi kufikia Shilingi bilioni 1.284 mwaka 2019/20 ikiwa ni ongezeko la asilimia 267. Hata hivyo, Kaimu Mhifadhi Mfawidhi wa HIBAMA Bw. Mohamed Shamte amebainisha kuwa, endapo vikwazo hivyo vya Halmashauri ya Wilaya vitadhibitiwa wanao uwezo wa kukusanya kati ya shilingi bilioni 40 hadi 60 kwa mwaka. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Bw. Eric Mapunda kwa upande wake amekanusha kuwepo kwa mgogoro huo na kusisitiza kuwa halmashauri yake imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa miujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia halmashauri hiyo.

Mkuu wa Wilaya Mhe. Ntemo hata hivyo baada ya kuhoji kuhusu uwepo wa tofauti hizo aliarifiwa kuwa suala hilo tayari lilikwishafikishwa ngazi mbali mbali za juu zaidi kwa hatua stahiki. Hata hivyo, ili kujiridhisha, DC Ntemo aliagiza kuundwa kwa Timu ya Wataalam kutoka pande hizo mbili ili wawasilishe maeneo yote yenye vipengele vinavyo kinzana ili kujiridhisha na kuchukua hatua muafaka mapema.

“Haiwezekani kuona vyombo viwili vya serikali vikaendelea kulumbana na kusababisha upotevu mkubwa wa mapato wakati vyombo hivyo vimeundwa kwa mujibu wa sheria na vinafahamu mipaka yake, hali hii haivumiliki hivyo ni wajibu wetu kuona hatua zinachukuliwa mapema iwezekanavyo kuinusuru hifadhi hii lakini pia kuokoa mapato ambayo yamekuwa yakipotea tangu kuanza kwa mzozo kati ya taasisi hizo mili” alisisitiza DC Ntemo.


Kaimu Mhifadhi Mfawidhi wa HIBAMA Bw. Mohamed Shamte (aliyesimama) akiwasilisha taarifa kwa Mkuu wa Wilaya Eng. Martin Ntemo ambaye alifuatana na Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Arch. Edwin Mapunda (aliyekaa kulia kwa DC) walipoitembelea taasisi hiyo kama sehemu ya ratiba ya kutembelea taasisi zinazofanya shughuli zake katika kisiwa cha Mafia.

10 views
RECENT POST