• raymhtz2

MAWAZIRI WAKAGUA UWEKEZAJI MKUBWA WA UTALII KATIKA KISIWA CHA MAFIA

Mawaziri watatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni walitembelea kisiwa cha Shungimbili kilichopo katika wilaya ya Mafia mkoani Pwani ili kujionea uwekezaji mkubwa wa hoteli ya kifahari ya Thanda ambayo imejikita katika shughuli za utalii na uhifadhi wa bahari. Uwekezaji huo umeweza kukuza thamani ya kisiwa hicho kiasi cha kufikia gharama ya kulala katika hoteli hiyo hufikia dola za Kimarekani 25,000 ambazo ni zaidi ya Shilingi milioni hamsini kwa siku moja.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji Mhe. Geofrey Mwambe na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, hivi karibuni walitembelea kisiwa cha Shungimbili wakiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Alhaj Abubakar Kunenge katika ziara ya kikazi kujiridhisha endapo uwekezaji wa hoteli hiyo ya Thanda umezingatia sheria za nchi na kwamba Serikali inakusanya kodi na tozo mbali mbali inavyostahili.

Hoteli hiyo ya kimataifa ya kitalii imejengwa katika kisiwa cha Shungimbili chenye ukubwa wa ekari nne tu lakini huduma zinazotolewa hapo ni za kiwango ambacho kinatambulika kimataifa cha nyota tano. Hoteli hiyo yenye uwezo wa kuchukua wageni kumi na nane kwa wakati mmoja kina huduma ya helikopta na mashua za kifahari pamoja na huduma nyingine nyingi ikiwemo michezo ya baharini na uzamiaji kwa ajili ya kujionea utajiri wa viumbe na mimea adimu ambavyo vinapatikana katika eneo hilo ambalo ni la kipekee duniani.

Mawaziri hao hata hivyo, wakati wakionesha kuridhishwa kwao na uwekezaji huo wameelekeza halmashauri ya Wilaya Mafia pamoja na taasisi zinazohusika na masula ya uwekezaji pamoja na uhifadhi wa bahari kuendelea kufuatilia kwa karibu shughuli na huduma ambazo zinatolewa kisiwani hapo ili kuhakikisha kuwa maslahi ya taifa pamoja na masuala mengine ya kiusalama yanazingatiwa na kusimamiwa ipasavyo.DC wa Mafia Eng. Martin Ntemo akiwaongoza Mawaziri na watendaji mbalimbali ikiwemo kamati ya ulinzi na usalama kukagua na kujionea uwekezaji mkubwa wa wa hoteli wilayani Mafia mkoani Pwani.

63 views
RECENT POST