• raymhtz2

MAFIA IKO TAYARI KWA UWEKEZAJI MKUBWA KATIKA SEKTA YA UTALII – LUKUVI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amejikuta akishikwa na mshangao kwa jinsi kisiwa cha Mafia kilivyojaaliwa fukwe nzuri za bahari lakini hazijatangazwa ipasavyo ili kuvutia uwekezaji hasa katika sekta ya utalii.

“Sikutarajia kukuta vivutio vizuri kama hivi hasa kwa upande wa fukwe ambazo zimeambaa eneo kubwa la kisiwa pamoja na ardhi ambayo ni kubwa na ikipangwa kimkakati itakaribisha wawekezaji wengi wakubwa kuwekeza katika kisiwa hiki tulivu” alisema Mhe. Lukuvi.

Kisiwa cha Mafia ni kisiwa cha tatu kwa ukubwa hapa nchini kikiunda moja ya wilaya saba za mkoa wa Pwani. Kisiwa hiki kina ukubwa wa kilometa za mraba 972 ambazo kati yake kilometa za mraba 407 ni nchi kavu na kilometa za mraba 565 ni eneo la maji. Katika kisiwa hiki kuna wakazi wapatao 53,083 ambao wanajishughulisha na shughili za uvuvi, kilimo hasa minazi na korosho na vilevile wanajishughulisha na shughuli za utalii. Kisiwa cha Mafia ni maarufu sana duniani kwa utalii wa viumbe na mimea iliyoko baharini.

Ziara hii ya Waziri Lukuvi imefanyika mara baada ya kuahirishwa kwa Mkutano wa 3 wa Bunge la 12 (bunge la bajeti) mwishoni mwa mwezi Juni, 2021. Kwa kipindi cha mwezi Julai Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amekuwa katika ziara ya kutatua kero za ardhi katika wilaya mbali mbali mkoani Pwani akitangaza kampeni maalum aliyoiita ‘Tokomeza Kero’. Kampeni hiyo ndiyo iliyomfikisha wilayani Mafia ambako kumekuwa na migogoro ya muda mrefu ya ardhi iliyohusu zaidi maeneo makubwa yanayomilikiwa na watu ama kampuni binafsi yakiwa katika mgongano na wananchi wanaoishi katika vijiji jirani na maeneo hayo.

Katika ziara hiyo kisiwani Mafia, Mhe. Lukuvi alifika pia kukagua mashamba makubwa yanayolalamikiwa katika kijiji cha Gonge kwenye mashamba ya Utumaini (ekari 4,040) na Kigomani (ekari 670) ambayo mmiliki wake yuko katika hatua za kupata wabia wa kuwekeza kwenye eneo hilo. Waziri Lukuvi baada ya kusikiliza pande zote zinazohusika na mgogoro huo akaielekeza Halmashauri ya Mafia kupitia nyaraka za umiliki wa maeneo hayo kwa umakini kabla ya kumshauri hatua za kuchukua. Akiwa katika maeneo hayo ya Gonga Mhe. Lukuvi alipata fursa ya alijionea fukwe nzuri za bahari zikiwa hazina mkakati mahsusi wa kuvutia uwekezaji mkubwa hasa kwa upande wa sekta ya utalii na kusisitiza kuwa ni budi halmashauri kuchangamkia fursa hiyo na kuhakikisha fursa hiyo inafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo.

Waziri Lukuvi alihitimisha ziara yake wilayani Mafia kwa mkutano mkubwa uliofanyikia katika eneo la Kilindoni ambako kero mabli mbali zilitolewa na kupatiwa majawabu.


Kutoka kusoto pichani ni DC wa Mafia Eng. Martin Ntemo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu - Uwekezaji Mhe. Geofrey Mwambe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, hivi karibuni walipotembelea kisiwa cha Shungimbili wakiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Alhaj Abubakar Kunenge wa kwanza kulia.


5 views
RECENT POST