• By Humphrey Makussa

MOTO WATEKETEZA OFISI YA MWENYEKITI WA MTAA


Ofisi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Miyombo katika Kata ya Misugusugu iliyoko Kibaha mkoani Pwani, imeteketea kwa moto siku ya Jumamosi ya tarehe 19 Desemba, 2020. Chanzo cha ajali hiyo bado kinaendelea kuchunguzwa ambapo taarifa za awali za Jeshi la Zimamoto zinaelezea kuwa moto huo uligunduliwa na majirani saa 8:00 za usiku.


Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Pwani Inspekta William Makyao ameelezea kuwa jitihada za majirani kuuzima moto huo zilishindikana wakati jeshi hilo likiwa njiani klutokea Kibaha kuelekea eneo la tukio mara baada ya kupokea taarifa kuhusu moto huo.


Hivyo, hadi Jeshi la Zimamoto lilipofika eneo hilo lilikuta tayari jengo limekwishaungua kwa kiwango kikubwa. Moto huo hata hivyo uliweza kudhibitiwa na kuzimwa kabla ya kusababisha madhara katika nyumba za jirani. Hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kufariki katika ajali hiyo.


Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Eng. Martin Ntemo alifika katika eneo husika ambapo baada ya kujionnea uharibifu uliotokana na moto huo alimuagiza Mkuu wa Polisi (OCD) wa Kibaha kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina unafanyika katika kipindi kifupi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.


“Ninawaelekeza Jeshi la Polisi Kibaha kwa kushirikiana na Jeshi la Zimanoto, mhakikishe uchunguzi wa kina unafanyika na kutoa matokeo mapema iwezekanavyo ili hatua kali zichukuliwe endapo itabainika kuwepo kwa uzembe au hujuma ya aina yoyote ile” alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya ya Kibaha huku akiongeza kuwa haiwezekani mali ya umma tena pamoja na nyaraka mbali mbali muhimu zinateketea kienyeji hivyo, ni lazima tutoe fundisho kwa tukio hili.Mkuu wa wilaya ya Kibaha (Kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Inspekta wa jeshi la zimamoto na uokoaji William Makyoo mara baada ya kutembelea Ofisi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Miyombo iliyoungua moto.

Ofisi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Miyombo ionekanavyo kwa upande wa mbele baada ya kuungua moto.


Ofisi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Miyombo ionekanavyo kwa upande wa mbele baada ya kuungua moto.


26 views
RECENT POST